Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baada ya kuweza kuokoa majeruhi, watoa huduma wabubujikwa machozi-WHO

Baada ya kuweza kuokoa majeruhi, watoa huduma wabubujikwa machozi-WHO

Wafanyakazi wa usaidizi wa kibinadamu wameelezea yale waliyoshuhudia tangu kuanza kwa operesheni ya kuhamisha majeruhi na wagonjwa kutoka Aleppo tarehe 15 mwezi uliopita.

Shirika la afya duniani, WHO limemnukuu mfanyakazi mmoja akisema kuwa mara baada ya kupata kibali cha kuingia Aleppo na kuhamisha wagonjwa, walianza kazi saa 11 alfajiri ambapo walichukua wagonjwa na kuwapeleka vituo vya afya.

Amesema timu zote na magari ya wagonjwa yalikuwa tayari katika eneo la makutano kutoka mashariki mwa Aleppo hadi Gaziantep.

Mfanyakazi huyo amesema walisuburi kwa zaidi ya saa kumi hadi saa tisa alasiri ndipo wakaelezwa kuwa msafara wa kwanza ulikuwa njiani kufika eneo lao la makutano.

Amesema alipoona gari la kwanza la wagonjwa yeye na wenzie walianza kutokwa na machozi na kutoamini kuwa uokoaji huo umekuwa wa kweli, kwani ni jambo ambalo wamesubiri kwa hamu kwa muda wa miezi mitatu.

Kuendelea kwa mapigano mashariki mwa Aleppo tangu Julai mwaka jana kumesababisha maelfu ya watu kujeruhiwa na wengine kuuawa, na hii imesababisha raia wakose huduma muhimu, ikiwa ni pamoja huduma za afya.