Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utapiamlo waathiri watoto milioni 1.3 Afghanistan

Utapiamlo waathiri watoto milioni 1.3 Afghanistan

Hali mbaya ya kibinadamu nchini Afghanistan imesababisha watu milioni 1.8 nchini humo wahitaji tiba dhidi ya utapiamlo uliokithiri.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu, OCHA imesema kati yao hao, zaidi ya milioni 1.3 ni watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano.

OCHA inasema kuwa mzozo unaoendelea nchini Afghanistan bado umesababisha nchi hiyo kuwa moja ya nchi hatari zaidi duniani na kwamba pamoja na idadi hiyo ya wenye utapiamlo, idadi ya watu wanaohitaji misaada nayo imeongezeka kwa asilimia 13 mwaka huu wa 2017 na kufikia milioni 9.3.

Makadirio ya hivi karibuni yaonyesha kuwa zaidi ya watu milioni 9 hawapati huduma muhimu za afya au hata wanapopata hazikidhi mahitaji.

Ripoti hiyo imesema kuwa uwiano wa vifo vya watoto wachanga na wanawake imebaki kuwa ya juu zaidi duniani.