Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rais wa zamani Ureno afariki dunia, Guterres atuma rambirambi

Rais wa zamani Ureno afariki dunia, Guterres atuma rambirambi

Rais wa zamani wa Ureno Mário Soares amefariki dunia hii leo akiwa na umri wa miaka 92.

Kufuatia taarifa hizo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres ametuma salamu za rambirambi kwa serikali ya Ureno, wananchi na familia ya marehemu huku akielezea kuhuzunishwa na kifo hicho.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imemnukuu Katibu mkuu akisema Bwana Soares ameacha pengo kubwa la  kisiasa kutokana na uimara na ujasiri wake na uzingatiaji wa kanuni na maadili wakati wa uhai wake.

Amesema Soares ambaye alikuwa Rais wa Ureno kuanzia mwaka 1986 hadi 1996, atakumbukwa kwa jinsi alivyowezesha kushamiri kwa demokrasia, uhuru na heshima kwa haki za msingi katika miongo ya hivi karibuni.

Bwana Guterres amesema mchango wa Soares umevuka mipaka ya Ureno siyo tu kwa jinsi alivyoimarisha ushirikiano wa Ureno kimataifa, bali kwa jinsi alivyoheshimu misigi ya uhuru na demokrasia, mambo ambayo yanamfanya awe mmoja wa viongozi shupavu kisiasa barani Ulaya na kimataifa.