Skip to main content

GBV yaangaziwa magharibi mwa Afghanistan

GBV yaangaziwa magharibi mwa Afghanistan

Kampeni dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia, GBV ilikuwa kitovu cha harakati za uhamasishaji zilizoendeshwa na Umoja wa Mataifa nchini Afhganistan mwaka 2016.

Kampeni za upashaji habari zilifanyika kwenye maeneo ya magharibi ya Herat, Ghor, Badghis na Farah ambapo mathalani mwezi Novemba mwaka jana ujumbe Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, UNAMA ulitumia njia tofauti ikiwemo majadiliano kwenye televisheni, radio na mikusanyiko ya umma.

Afisa wa haki za binadamu na ujumbe huo anayefanya kazi katika ukanda wa magharibi Sia Mawalla amesema nia ya kampeni hiyo ilikuwa kuleta pamoja makundi mbalimbali ya wanawake, wasichana, wanaume, wavulana, viongozi wa serikali na wanaharakati ili kuongeza uelewa wa madhara ya unyanyasaji dhidi ya wanawake kijamii, na kimaendeleo.

Ripoti za maeneo hayo zinaonyesha kuwepo kwa zaidi ya kesi 600 zinazohusu ndoa za kulazimishwa, ubakaji, mauaji na kuathirika kisaikolojia kwa wanawake ambao tayari wamejiandikisha kwenye idara ya polisi na taasisi za kisheria.

Wakati wa moja ya mijadala hiyo huko Herat, viongozi 13 wa kidini walitangaza kuwa ukatili dhidi ya wanawake hauendani na maadili ya Kiislamu.