Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sitisho la mapigano Syria halijafanikisha ufikishaji misaada

Sitisho la mapigano Syria halijafanikisha ufikishaji misaada

Mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa Jan Egeland amesema sitisho la mapigano huko Syria bado halijatoa fursa ya kutosha kuweza kufikisha misaada ya kibinadamu kwa wahusika.

Akizungumza na waandishi wa habari huko Geneva, Uswisi hii leo, Bwana Egeland amesema kwa mwezi wa Januari, Umoja wa Mataifa haujapata ruhusa ya kufikisha misaada kwenye maeneo matano kati ya 21, hasa katika maeneo ya vijijini ya mji mkuu Damascus, Homs na Hama.

(Sauti ya Egeland)

“Bado haijaisha, ijapokuwa sitisho la mapigano linazingatiwa kwenye maeneo mengi Syria, kuna kizungumkuti kinakumba raia na tunashindwa kupata ruhusa kufika maeneo mengi.”

Naye mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Syria Staffan de Mistura amesema ni matumaini yake kuwa mazungumzo baina ya pande kinzani nchini Syria yanayotarajiwa kufanyika huko Kazakhstan yanaweza kumaliza kabisa mapigano.

Sitisho hilo la mapigano liliratibiwa na Urusi na Uturuki, na kuungwa mkono na Baraza la Usalama kupitia azimio namba 2236.

De Mistura amesema tayari Urusi na Uturuki zimetoa hakikisho la kufanyika kwa mashauriano hayo Kazakhstan ambayo Umoja wa Mataifa utashiriki na hivyo…

(de Mistura)

“Msimamo wetu ni kwamba hatua kama hizi zinapaswa kuungwa mkono na ni matumaini yetu kuwa yatafanikiwa na ni bila shaka zinaungwa mkono.”