Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wafanyakazi 4 wa UM Colombia wafukuzwa kazi kwa kukiuka maadili

Wafanyakazi 4 wa UM Colombia wafukuzwa kazi kwa kukiuka maadili

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Colombia, hii leo umetangaza kuwafukuza kazi, waangalizi wake watatu wa mkataba amani nchini humo pamoja na msimamizi wao kwa kukiuka maadili. Grace Kaneiya na ripoti kamili.

(Taarifa ya Grace)

Taarifa ya ujumbe huo kutoka mji mkuu wa Colombia, Bogota, imesema hatua hiyo inafuatia uchunguzi uliofanywa wa hali ilivyokuwa wakati wa sherehe za mkesha wa mwaka mpya kwenye kituo cha muda cha waasi wa zamani wa FARC-EP ambako waangalizi hao walishiriki.

Hatua hii inakuja baada ya kuripotiwa kuwa watendaji hao walishiriki dansi na wasichana wa kikundi hicho, wakati huu ambapo Umoja wa Mataifa unasimamia utekelezaji wa mkataba wa amani kati ya serikali ya Colombia na waasi hao wa zamani.

Umoja wa Mataifa umesisitiza azma yake ya kusimamia kutopendelea upande wowote katika utekelezaji wa vipengele vya mkataba ikiwemo sitisho la mapigano, kumaliza uhasama na kusalimisha silaha.