Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matumbawe kukumbwa na uharibifu ikiwa hatua hazitachukuliwa

Matumbawe kukumbwa na uharibifu ikiwa hatua hazitachukuliwa

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa mazingira UNEP, limeonya kwamba ikiwa uchafuzi wa bahari unaosababishwa na mabadiliko ya tabianchi utaendelea, asilimia 99 ya matumbawe duniani yataathirika kwa kuwa meupe.

Kwa mujibu wa UNEP, upunguzaji wa hewa chafuzi unaweza kuyapa matumbawe wastani wa miaka 11 zaidi kabla ya kukabiliwa na uharibifu huo na kwamba kutabiri kiwango kikubwa cha weupe na kuazimia kuchukua hatua kwaweza kusaidia uhifadhi.

Mfumo mpya wa utabiri wa hali ya hewa duniani unaonyesha ni matumbawe gani yatakayoshambuliwa awali na weupe, hatua inayotishia mazingira imesema UNEP katika taarifa yake.

Utafiti uliofanywa na shirika hilo la mpango wa mazingira unaonyesha kuwa matumbawe yaliyo nchini Taiwan, maeneo ya Uturuki na visiwa vya Caicos ni miongoni mwa yatakayoshuhudia weupe katika mwaka huku mengine katika nchi kama vile pwani ya Bahrain, Chile na visiwa vya Polynesia nchini Ufaransa yatashambuliwa karne zijazo.