Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kikundi kingine DRC chajiunga na mkataba wa amani

Kikundi kingine DRC chajiunga na mkataba wa amani

Huko nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC, jukwaa la kuheshimu katiba ya nchi hiyo limetangaza hii leo kuwa litatia saini makubaliano ya kisiasa yaliyotokana na mashauriano yaliyoratibiwa na jumuiko la maaskofu nchini humo, CENCO.

Mratibu wa jukwaa hilo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama cha MLC Eve Bazaïba, amesema hayo leo baada ya mkutano na viongozi wa CENCO huko Kinshasa.

Bi. Bazaïba amesema wamefikia hatua hiyo baada ya wasuluhishi kutambua madai yao, akieleza kuwa hoja yao ni kushika madaraka lakini kwa mujibu wa katiba na si vinginevyo.

Kitendo cha jukwaa hilo kukubali kujumuika kwenye makubaliano hayo yaliyopitishwa tarehe 31 mwezi uliopita kinaendeleza wito wa Umoja wa Mataifa wa kutaka pande zote kinzani huko DRC kushiriki kwenye mchakato huo kwa maslahi ya wananchi wote.