Skip to main content

Watu takriban milioni 1.2 huko Cameroon wanahitaji msaada wa dharura: OCHA

Watu takriban milioni 1.2 huko Cameroon wanahitaji msaada wa dharura: OCHA

Umoja wa Mataifa, Serikali ya Cameroon na mashirika yasiyo ya kiserikali wamezindua ombi la dola milioni 310 ili kutekeleza mpango wa usaidizi kwa watu takriban milioni 1.2 kwenye mikoa ya kaskazini na mashariki mwa nchi hiyo wakati huu ambapo inaendelea kukabiliana na mgogoro wa usalama ulioathiri vipato vya mamilioni ya watu.

Kwa mujibu wa Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini humo ambaye pia ni mratibu wa misaada ya kibinadamu katika ofisi ya kuratibu misaada kibinadamu OCHA, Najat Rochdi, tayari serikali na watu wa Cameroon wameonyesha ukarimu mkubwa kwa mamia ya maelfu ya wakimbizi kutoka Nigeria na Afrika ya Kati.

Bi Rochdi ametoa wito kwa washirika wa kibinadamu na wafadhili wa kimataifa kusaidia wale wanaohitaji msaada zaidi.

OCHA inasema kuwa katika mwaka huu wa 2017, watu karibu milioni tatu nchini Cameroon wanahitaji misaada. Karibu milioni 2.6 watakabiliwa na uhaba wa chakula, wengi wao wakiwa katika maeneo kame ya ukanda wa Sahel wa mikoa ya kaskazini. Utapiamlo bado uko juu na unawaakithiri baadhi ya watoto 200,000.