Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko Haiti kwa kumpata Rais- MINUSTAH

Heko Haiti kwa kumpata Rais- MINUSTAH

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Haiti, Sandra Honoré amesema wametambua chapisho la mwisho la matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika nchini humo tarehe 20 mwezi Novemba mwaka jana.

Bi. Honoré ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Haiti, MINUSMAH, amesema wao na wadau kama vile mabalozi wa Brazil, Canada, Ufaransa, Hispania, Marekani na Muungano wa Ulaya nchini humo wamempongeza rais mteule Jovenel Moïse.

(Sauti ya Bi. Honoré )

"Kitendo cha Baraza la uchaguzi Haiti kumthibitisha Bwana Jovenel Moïse kuwa Rais mteule wa Haiti, nchi hii sasa ina fursa ya kurejea kwenye utawala wa kisheria na kuwa na kiongozi wa taifa aliyechaguliwa kidemokrasia, kuwa na bunge ambalo litaendelea kufanya kazi kama vile mabunge yanapaswa kuwajibika katika ujenzi wa demokrasia.”

Bi. Honoré amesema sasa ni fursa kwa Rais mteule kuapisha serikali mpya na wanachi wa Haiti na wadau wa maendeleo na kisiasa Haiti kushughulikia changamoto zinazokabili nchi hiyo.

Ametaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na zile za kiuchumi, kiafya, tabianchi na uhakika wa chakula.

Halikadhalika amesema Umoja wa Mataifa na wadau hao wanasubiri kwa hamu kuapishwa kwa Rais mteule wa Haiti, tarehe 7 mwezi ujao na hatimaye kushirikiana kwa maslahi ya wananchi wa Haiti.