Skip to main content

UNSOM yakaribisha ari ya kuleta maelewano Gaalkacyo

UNSOM yakaribisha ari ya kuleta maelewano Gaalkacyo

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko Somalia, Michael Keating amekaribisha makubaliano ya hii leo kati ya marais Abdiweli Mohamed Ali "Gaas" wa jimbo la Puntland na Abdikarim Hussein Guled wa Galmudug yenye lengo la kujenga amani na kuaminiana huko Gaalkacyo.

Marais hao wa majimbo hayo wamekubaliana juu ya masuala matatu, ikiwemo ukomeshaji wa uhasama katika Gaalkacyo na kujenga imani kati ya maeneo hayo mawili.

Makubaliano hayo ni pamoja na uondoaji wa majeshi kutoka maeneo yenye mzozo huo mjini Gaalkacyo na vikosi kurejea kwenye maeneo yao, pili, kuondolewa kwa vizuizi vyote vya barabarani vilivyowekwa huko Puntland na Galmudug ili kuruhusu usafirishaji huru wa watu.

Halikadhalika utekelezaji wa mafunzo ya pamoja ya polisi wote wa Kaskazini na Kusini mwa Gaalkacyo na kuimarisha usalama, na kujenga imani na ushirikiano kati ya majimbo hayo mawili.

Viongozi hao wamekubaliana kukutana baadaye mwezi huu kusaidia utekelezaji wa makubaliano hayo.

Kwa mantiki hiyo, Keating ambaye pia ni Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa Somalia, UNSOM amesema hatua hiyo ni muhimu kwa ajili ya kuruhusu mchakato wa kutatua masuala hayo ambayo yamesababisha migogoro na itajenga amani ya kudumu.