Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

António Guterres; Fahamu wasifu wake

António Guterres; Fahamu wasifu wake

António Guterres, Katibu Mkuu wa tisa wa Umoja wa Mataifa anaanza kazi rasmi leo tarehe Mosi mwezi 2017.

Akiwa ameshuhudia machungu mengi ya watu walio hatarini zaidi duniani, kwenye kambi za wakimbizi na kwenye vita, Katibu Mkuu ameazimia kuweka utu wa kibinadamu kuwa msingi wa kazi yake na kuhudumu kama mleta amani, mjenzi wa daraja na mwendelezaji wa marekebisho na ubunifu.

Kabla ya kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu, Bwana Guterres alikuwa Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR kuanzia mwezi Juni mwaka 2005 hadi Disemba 2015, akiongoza moja ya mashirika ya kibinadamu wakati wa kipindi kilichoshuhudia kiwango kikubwa cha wakimbizi katika miongo kadhaa. Mapigano nchini Syria na Iraq na majanga huko Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Yemen, yalisababisha kuongezeka kwa operesheni za UNHCR kwa kuwa idadi ya watu waliokimbia makwao kutokana na mizozo na mateso iliongezeka kutoka milioni 38 mwaka 2005 hadi zaidi ya milioni 60 mwaka 2015.

image
Akiwa Waziri mkuu wa Ureno, Guterres akiwa na kiongozi wa Timor Mashariki Xanana Gusmão baada ya kufanikisha harakati za kimataifa za kumaliza mzozo wa nchi hiyo. (Picha: LUSA Antonio Cotrim)
Kabla ya kujiunga na UNHCR, Bwana Guterres alihudumu serikalini na utumishi wa umma kwa zaidi ya miaka 20. Alikuwa Waziri Mkuu wa Ureno kuanzia mwaka 1995  hadi 2002, kipindi ambacho alihusika zaidi na jitihada za kimataifa za kusaka suluhu ya mzozo wa Timor ya Mashariki.

Akiwa Rais wa Baraza la Ulaya mapema mwaka 2000, aliongeza kupitishwa kwa ajenda ya Lisbon kuhusu ukuaji uchumi na ajira, akiwa mwenyekiti mwenza wa mkutano wa kwanza wa pamoja wa Ulaya na Afrika. Alikuwa mjumbe wa baraza la kitaifa la Ureno kuanzia mwaka 1991 hadi 2002.

Bwana Guterres alichaguliwa kwenye bunge la Ureno mwaka 1976 na kuhudumu kwa miaka 17. Wakati huo alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Uchumi, Fedha na Mipango, na baadaye Kamati ya Bunge kuhusu Utawala wa Majimbo, Manispaa na Mazingira. Halikadhalika alikuwa kiongozi wa kundi la chama chake bungeni.

Kuanzia mwaka 1981 hadi 1983, Bwana Guterres alikuwa mjumbe wa mkutano wa mabunge ya Ulaya, ambako aliongoza Kamati ya Demografia, Uhamiaji na Wakimbizi.

Kwa miaka mingi Bwana Guterres amejihusisha na Socialist International, shirika la kimataifa la vyama vya kisiasa vyenye mrengo wa demokrasia ya kijamaa ambapo alikuwa Makamu Mwenyekiti kuanzia mwaka 1992 hadi 1999, akiwa mwenyekiti mwenza wa Kamati ya Afrika na baadaye Kamati ya Maendeleo kuanzia mwaka 1999 hadi katikati ya mwaka 2005. Halikadhalika alikuwa muasisi wa Baraza la wakimbizi la Ureno na pia chama cha walaji Ureno, DECO. Amekuwa pia Rais wa Centro de Acção Social Universitário, ambacho ni chama kilichohusika na miradi ya maendeleo kwenye makazi duni huko Lisbon mwanzoni mwa miaka ya 1970.

Bwana Guterres ni mjumbe wa Klabu ya Madrid, ambacho ni kikundi cha Marais na Mawaziri Wakuu wastaafu kutoka nchi mbali mbali duniani.

image
Wakati akiwa Kamishna Mkuu wa UNHCR alitembelea kambi za wakimbizi na hapa ni alipokutana na viongozi wa jamii ya kisomali kwenye kambi ya wakimbizi ya Hagadera karibu na Dadaab, nchini Kenya. (Picha: UNHCR/Evelyn Hockstein)
Bwana Guterres alizaliwa huko Lisbon, Ureno mwaka 1949 na alihitimu taasisi ya juu ya ufundi, Instituto Superior Técnico na kutunukiwa shahada ya uhandisi. Anazungumza kwa ufasaha Kireno, Kiingereza, Kifaransa na Kispanyola. Mke wake ni Catarina de Almeida Vaz Pinto, Naibu Meya wa masuala ya Utamaduni mjini Lisbon, na ana watoto watatu na wajukuu watatu.