Skip to main content

Baraza la usalama lipitisha azimio la kusitisha uhasama Syria.

Baraza la usalama lipitisha azimio la kusitisha uhasama Syria.

Baraza la usalama limepitisha kwa kauli moja azimio namba 2336 linalolenga usitishwaji wa mapigano Mashariki ya kati hususani nchini Syria.

Katika kikao chake cha mwisho hii leo kwa mwaka 2016, baraza limezingatia maazimio yaliyotangulia ya mwaka jana na mapema mwaka huu, kuhusu hali nchini Syria.

Azimio hilo lilipendekezwa na Urusi na Uturuki.

Akizungumza wakati wa kupitisha azimio hilo Naibu Mwakilishi wa kudumu wa Marekani katika ofisi za Umoja wa Mataifa Balozi Michele Sison anaeleza kwanini wameunga mkono azimio.

(Sauti Balozi Michele)

 ‘‘Tumelipigia kura ya ndio azimio hili kwasababu lina uwiano sahihi,  matumaini ya tahadhari na usaidizi.  Tungependa kuangazia mambo muhimu mawili,  tumaini letu kuwa sitisho la mapigano litasalia . Kutokana na hili tunasikitishwa na ripoti za ukatili unaungwa mkono na wanamgambo wa Hezbolla huko Wadi Barada. Kupitishwa kwa azimio hili iwe ishara kwamba vitendo kama hivyo lazima visitishwe.’’

Kwa upande wake mwakilishi wa kudumu wa Urusi katika ofisi za Umoja wa Mataifa Balozi Vitally Churkin amesema sasa ni muda wa vitendo kwani miaka sita ya vita imetosha.

Akiongea kupitia mtafsiri kwa lugha ya Kingereza Balozi Curkin amesma .

( Sauti Balozi Churkin)

‘‘Hebu tufanye kazi kwa kumaanisha , ili kuhakikisha mwaka 2017  tunafanikisha utulivu wa kisiasa nchini Syria. Ikiwa jumuiya ya kimataifa itafanya kazi wakiongozwa na hii dhamira, maslahi ya watu wa Syria, na utulivu wa ukanda mzima,  tunaweza  kupata mafanikio.’’

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekaribisha azimio hilo akisema ana matumaini azimio litasukuma majadiliano ya kusaka suluhu yanayotarajiwa kufanyiaka Februari 8,2017.