Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban aaga akisema atasalia mtoto wa Umoja wa Mataifa

Ban aaga akisema atasalia mtoto wa Umoja wa Mataifa

Nats..

Hivyo ndivyo ilivyokuwa majira ya saa sita mchana siku ya Ijumaa kwa saa za New York, Marekani ambapo Katibu Mkuu wa nane wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon aliaga rasmi wafanyakazi wa umoja huo baada ya kuhudumu kwa miaka 10.

Awamu mbili za miaka mitano na kufanya jumla miaka kumi, zikimwezesha kusafiri maeneo mbali mbali ya ulimwengu kushuhudia madhila yanayokumba wananchi sambamba na mafanikio ya kazi za Umoja wa Mataifa.

Ijumaa akatoa shukrani zake kwa wafanyakazi akisema maneno yake ni mawili tu asante sana na zaidi ya hapo..

(sauti ya Ban)

“Kamwe msikate tamaa, endelezeni ndoto zenu na endelee kuamini na kufanya kazi kwa bidii hadi pale mnapopata mafanikio.”

Na akaelezea kile alichofanya..

(sauti ya Ban)

“Kwa miaka kumi iliyopita, nimekuwa nafanya kazi kupata sauti kwa wasio na sauti. Mtetezi wa wasioweze kujitetea. Lakini mnapaswa kuendeleza suala hilo.”

Ban akaenda mbali zaidi kuzungumzia jukumu lake la mwisho akiwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa tarehe 31 Disemba 2016 la kuangusha kitufe kutoka jengo moja huko Times Square jijini New York akisema.

(Sauti ya Ban)

“Najiona kidogo kama Cinderella. Kesho usiku wa manane kila kitu kinabadilika.”

Ban akasema kuwa hatokuwa tena Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa lakini atakuwa anajivunia kubeba jina la raia wa kimataifa na kwamba atakuwa Balozi mwema na siku zote atasalia mtoto wa Umoja wa Mataifa.

Ban ambaye ni raia wa Jamhuri ya Korea ikitambulika pia kama Korea Kusini, alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa mwaka 2006 na hatimaye kuanza rasmi jukumu hilo tarehe Mosi Januari mwaka 2007, jukumu ambalo linafikia ukingoni tarehe 31 mwezi huu.