UM wakaribisha sitisho la mapigano kote Syria

29 Disemba 2016

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Staffan de Mistura amekaribisha tangazo lililotolewa hii leo la kuanza kwa sitisho la mapigano maeneo yote ya nchi hiyo.

Habari zinasema kuwa milio ya risasi na makombora nchini Syria itakoma kuanzia saa Sita usiku hii leo kwa saa za Syria likihusisha vikosi vya serikali na vikundi vilivyojihami nchini humo.

Katika taarifa yake mjumbe huyo maalum amesema sitisho kamili la mapigano na chuki miongoni  mwa pande kinzani ndio msingi wa mfumo  uliowekwa na azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa  namba 2254 la mwaka 2015.

Kwa mantiki hiyo amesema ni matumaini yake kuwa utekelezaji wa hatua hii utaokoa maisha ya raia na kuwezesha misaada ya kibinadamu kufikia wahitaji nchini Syria.

Bwana de Mistura amesema kwa mtazamo wako taarifa hizi za karibuni zinapaswa kuchangia kwenye mashauriano shirikishi na yenye matokeo chanya baina ya pande kinzani Syria, mashauriano ambayo yataitishwa chini ya Umoja wa Mataifa tarehe 8 mwezi Februari mwakani.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter