Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya umaskini na haki za binadamu Saudia Arabia kuangaziwa

Hali ya umaskini na haki za binadamu Saudia Arabia kuangaziwa

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu umaskini uliokithiri na haki za binadamu, Philip Alston, tarehe 8 mwezi ujao ataanza ziara ya wiki mbili nchini Saudi Arabia, lengo ikiwa ni kuangazia harakati za nchi hiyo kutokomeza umaskini na jinsi harakati hizo zinavyozingatia haki za binadamu.

Bwana Alston amenukuliwa akisema kuwa Saudi Arabia ni nchi tajiri, lakini kama ilivyo kwa nchi nyingine hali ya umaskini miongoni mwa raia ipo na hivyo ni vyema kuangaziwa kwa kuzingatia umaskini ni zaidi ya kukosa kipato.

Mathalani ametaja suala la ukosefu wa huduma za msingi na kutengwa kijamii masuala ambayo amesema akiwa nchini humo atayaangazia hususan mifumo ya hifadhi ya jamii na jinsi inaathiri maskini.

Ziara ya Alston nchini humo inafuatia mwaliko wa serikali ya Saudi Arabia ambapo atakutana na wawakilishi wa serikali, mashirika ya kiraia, wasomi na wanadiplomasia.

Mwishoni mwa ziara yake atazungumza na waandishi wa habari tarehe 19 mwezi Januari na hatimaye kuwasilisha ripoti ya matokeo ya ziara mbele ya Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa mwezi Juni mwakani.