Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuki dhidi ya wageni ikomeshwe: Eliasson

Chuki dhidi ya wageni ikomeshwe: Eliasson

Viongozi kote duniani wametakiwa kuacha hima kuwagawanya watu katika umimi na usisi, amesema Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson anayemaliza muda wake wa uongozi mwishoni mwa mwaka huu.

Bwana Eliasson ameshikilia nafasi hiyo ya pili kwa ukubwa katika shirika hilo kwa karibu kipindi cha miaka mitano huku akiwa pamoja na mambo mengine ameshiriki kikamilifu katika majadiliano ya malengo ya maendeleo endelevu yaliyofikiwa mwaka 2015.

Katika mahojiano na redio ya Umoja wa Mataifa Naibu Katibu Mkuu huyo ameelezea kile alichokiita safari ya ajabu na kuelezea namna chuki zinavyoweza kuzaa majanga duniani.

( Sauti ya Eliasson)

‘‘Ninatiwa hofu sana na huu mtindo wa kujitambulisha kinyume na wengine, ikiwa ni katika dini, koo, au kabila. Hii ina maana unadharau usawa wa kibinadamu kwa kuwa unazingatia kuwa sisi ni bora kuliko wao.’’

Amesema migawanyo na chuki hizo huzaa majanga makubwa duniani ambayo hutumia mabilioni ya dola katika usaidizi wa kibinadamu , operesheni za ulinzi wa amani na michakato ya kusaka suluhu.