Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa MONUSCO wa kuimarisha usalama Uvira DRC wazaa matunda

Mradi wa MONUSCO wa kuimarisha usalama Uvira DRC wazaa matunda

Mwezi mmoja tangu ujumbe wa Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO, uanzishe mkakati wa kuimarisha ulinzi wa raia, SOLIUV kwenye eneo la Uvira, jimbo la Kivu Kusini, hali ya usalama imeelezwa kuwa imeimarika.

Kanali Gilbert Serushago ambaye ni kamanda wa polisi wa taifa Uvira amesema SOLIUV imepunguza ukosefu wa usalama kwa zaidi ya asilimia 50 ambapo vifaa walivyopatiwa na MONUSCO vinarahisisha utendaji wao wa kazi, mathalani pikipiki.

Mradi huo unahusisha doria za pamoja kati ya polisi, raia na watendaji kutoka ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa ambapo wao wanatoa usaidizi wa vifaa ikiwemo magari, pikipiki, mlo kwa walio doria na vifaa vya mawasiliano.

Hata hivyo watendaji hao wamesihi kuwa mwaka ukifikia ukingoni hali inaweza kubadilika hivyo wameomba usaidizi zaidi kutoka MONUSCO sambamba na udhibiti wa vikundi vilivyojihami huko Uvira ambavyo ni kikwazo kwa mradi huo.