Uamuzi wa jukwaa la viongozi Somalia watia hofu

27 Disemba 2016

Umoja wa Mataifa pamoja na wadau wengine wa Somalia wameingiwa hofu na uamuzi wa hivi karibuni wa jukwaa la kitaifa la uongozi nchini humo, NLF kuhusu mchakato wa uchaguzi.

NLF iliamua kutupilia mbali hoja za kuwaondoa baada ya wagombea kwa misingi mbali mbali sambamba na kuongeza viti vya wabunge kwenye bunge la juu, kitendo ambacho Umoja wa Mataifa na wadau wake wanasema ni kinyume na katiba ya Somalia.

Wadau hao wamesema ingawa wanapigia chepuo uzinduzi wa bunge la kitaifa hii leo ikiwa ni hatua ya kusongesha mchakato wa uchaguzi, bado wanataka kuona mchakato wa Bunge la juu ukiendelea na viti 54 kwa mujibu wa katiba.

Wamesema mpango wowote wa kuongeza idadi ya viti vya bunge hilo usubiri baada kura ya rais kwenye bunge jipya na mpango huo uzingatia mchakato sahihi wa kikatiba.

Baadhi ya kasoro zilizotajwa pia na wadau hao ni NLF kushindwa kushughulikia visa vya baadhi ya viti vya wabunge vilivyotengwa kwa wanawake kutenguliwa na kuchukuliwa na wanaume.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter