WFP imo hatarini kusitisha msaada wa chakula CAR

WFP imo hatarini kusitisha msaada wa chakula CAR

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limetoa ombi la haraka la zaidi ya dola milioni 21 ili kuepuka janga la kibinadamu linalotishia maisha ya takriban watu 150,000 nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.

WFP inasema bila ya msaada huo, italazimika kusitisha usaidizi wa chakula nchini humo ifikapo mwezi Februari, ikisema fedha hizo zitatumika kununua tani 14,580 ya chakula.

Kutokana na upungufu wa fedha mwaka 2016, WFP haikuweza kuwasaidia nusu milioni ya watu ambao walikuwa katika hali mbaya.

Vile vile katika mwezi wa Novemba na Disemba, WFP iligawa chakula shuleni siku 15 badala ya 18 kama ilivyopangwa hapo awali.

Mapigano mapya katika mji wa Kaga Bandoro huko CAR yamezidisha ugumu wa maisha kwa maelfu ya watu wanaolazimika kujimudu na asilimia 25 ya resheni nzima ya chakula.