Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 10 ya uongozi wangu umenifungua mengi- Ban

Miaka 10 ya uongozi wangu umenifungua mengi- Ban

Baada ya miaka 10 ya kuongoza Umoja wa Mataifa, mtendaji mkuu wa chombo hicho Ban Ki-moon anahitimisha jukumu hilo tarehe 31 mwezi huu wa Disemba.

Akizungumza kwenye mahojiano yake ya mwisho na Idara ya Habari ya Umoja wa Mataifa, Ban amesema ilikuwa ni heshima kubwa kwake yeye kuongoza taasisi hiyo katika muongo mmoja uliokabiliwa na changamoto lukuki ikiwemo mabadiliko ya tabianchi na mizozo akisema kile alichobaini...

(Sauti ya Ban)

“Kwa mtazamo wangu kama Katibu Mkuu wakati wa uongozi wangu nikishughulikia mizozo hapa na pale, nimeona kuwa migogoro haisababishwi na wananchi. Migogoro mingi kwa bahati mbaya inasababishwa na viongozi, kwa sababu viongozi wengi hawaonyeshi nia ya dhati kuzingatia malengo na misingi ya katiba ya Umoja wa Mataifa na haki za binadamu. Ndio maana wananchi wanakuwa na hasira na wanapinga uongozi wao.”

Amesema ndio maana amekuwa anasihi viongozi kuweka mbele maslahi ya umma akiwaeleza kuwa iwapo wangalikuwa na mshikamano na raia wao, mizozo ingalikuwa michache hivi sasa.

Na alipoulizwa baada ya kuhitimisha jukumu lake nini kitafuatia?

 (Sauti ya Ban)

 “Mimi ni mtu ambaye niko tayari kwa mawazo mapya. Kama Katibu Mkuu mstaafu bila shaka nimejifunza mambo mengi na maono na ufahamu. Chochote kitakachokuwa cha lazima, popote pale itakapokuwa lazima, sitasita kufanya jambo jema kwa nchi yangu au hata jamii ya kimataifa zaidi ya nchi yangu Korea. Nadhani hilo ni jambo jema kwa katibu mkuu mstaafu kupeleka usaidizi wake kwa jambo jema.”