Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mauzo ya nje kutoka LDCs kuongezeka iwapo zitapata soko G20

Mauzo ya nje kutoka LDCs kuongezeka iwapo zitapata soko G20

Nchi maskini zaidi duniani, LDCs zinaweza kuongeza kiwango cha biashara ya nje kwa asilimia 15 iwapo zitapata soko kwenye nchi zilizojikwamua kiuchumi, au G20.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD iliyochapishwa hii leo ikisema kuwa ingawa LDCs zinachangia asilimia 12 ya idadi ya watu duniani, kiwango cha mauzo ya bidhaa nje ya nchi ni asilimia moja tu.

Mkurugenzi wa UNCTAD wa masuala ya biashara ya nje, Guillermo Valles amesema licha ya maendeleo kibiashara duniani katika muongo uliopita bado ushiriki wa LDCs umesalia kidogo.

Hivyo amesema kuongeza maradufu ushiriki wao kwa mujibu wa lengo namba 17 la ajenda 2030 ni lazima kuondoa suala la ushuru wa bidhaa zinazouzwa G20, hatua ambayo itaongeza thamani ya biashara kwa dola bilioni 10 kwa mwaka.