Amani izingatiwe kwenye kipindi cha mpito DRC- Ban

21 Disemba 2016

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema anafuatilia kwa karibu hali inavyoendelea huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wakati huu ambapo usuluhishi unaoongozwa na mkutano wa kitaifa wa makanisa nchini huko CENCO umeanza tena hii leo.

Taarifa ya msemaji wake imemnukuu Katibu mkuu akizitaka pande zote zinazohusika katika upatanishi na usuluhishi kuafikiana kwa njia ya amani na kujaribu kutatua masuala yanayohusiana na mipango ya mpito kuelekea uchaguzi mkuu kwa mujibu wa katiba ya DRC.

Ban ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa kuweka mbele maslahi ya nchi na raia badala ya maslahi yao binafsi.

Amemsihi Waziri mkuu Samy Badibanga kuchukua hatua madhubuti kwa mujibu wa makubaliano ya kisiasa ya tarehe 18 Oktoba huku akisisitiza umuhimu wa vikosi vya usalama nchini humo kujizuia kuchukua hatua zinazoweza kusababisha vifo kama vilivyoripotiwa kwenye mji mkuu Kinshasa.

Ban amezitaka mamlaka kwa mara nyingine tena kukuza na kulinda haki za binadamu na kuzingatia uhuru wa kimsingi unaotajwa katika Katiba.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter