Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kauli za Duterte kuwa aliua watu zichunguzwe: Zeid

Kauli za Duterte kuwa aliua watu zichunguzwe: Zeid

Kamishna wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein ametoa wito kwa mamlaka ya mahakama ya Ufilipino kuzindua mchakato wa uchunguzi kufuatia tamko la wiki iliyopita la Rais Rodrigo Duterte wa Ufilipino kuwa wakati akiwa Meya wa Davao aliua watu na kushawishi watu wengine wafanye hivyo.

Rais Duterte alinukuliwa tarehe 14 mwezi huu akieleza kuwa wakati akiwa meya alifanya doria usiku kwa kutumia pikipiki na kuuawa watu ambapo alienda mbali zaidi na kuthibitisah kuua watu watatu.

Kamishna Zeid katika taarifa yake amesema vitendo kama hivyo ni kinyume na haki kwa mujibu wa katiba ya Ufilipino.

Halikadhalika mauaji hayo yalielezwa na Rais Duterte ni kinyume na sheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na haki ya kuishi, uhuru na kuepuka vurugu na haki ya mtu kulindwa na sheria.

Amesema itakuwa jambo la ajabu iwapo mamlaka za sheria Ufilipino hazitaanzisha uchunguzi dhidi ya mauaji hayo ambayo mwenyewe Rais Duterte amekiri kutekeleza.

Wakati huo huo Kamishna Zeid ameunga taarifa ya Ijumaa na mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa Agnes Callamard ay kutaka Ufilipino iondoe masharti yote iliyomwekea ili aweze kupata kibali cha kwenda nchini humo kuchunguza madai ya mauaji kinyume cha sheria ya wafanya biashara watuhumiwa wa madawa ya kulevya.