Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fidel Castro akumbukwa; Angola yasema atalia shujaa

Fidel Castro akumbukwa; Angola yasema atalia shujaa

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao maalum cha kumuenzi Fidel Castro, Rais wa zamani wa Cuba aliyefariki dunia tarehe 25 mwezi uliopita.

Wakati wa kikao hicho, wawakilishi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa walitoa hotuba kuwakilisha kanda wanazotoka au nchi zao, hotuba ambazo zilidhihirisha vile ambavyo hayati Fidel Castro aligusa nchi zao kwa njia mbali mbali iwe kiuchumi, kisiasa na kijamii.

(Nats)

Peter Thomson ambaye ni Rais wa Baraza Kuu alipatiwa heshima ya kuongoza kikao hicho kilichoitishwa na Cuba ambapo alisema ujasiri, ari na upendo aliokuwa nao Fidel Castro uliwezesha nchi yake kukabili na kuhimili changamoto zilizotokana na vikwazo vya kiuchumi dhidi yake, hivyo akasema..

(Sauti ya Thomson)

 “Tunavyoenzi maisha na kuhuzunishwa na kifo kiongozi huyu mwenye ushawishi mkubwa, tunapata faraja kwa ukweli kwamba maadili yake ya msingi ambayo ni mshimano, maenddeleo, amani haki na kuheshimiana yataendelea.”

Angola! Nchi ambayo Fidel Castro alipeleka wananchi wake kupigana dhidi ya waasi, iliwakilishwa na Balozi  Ismael Abraão Gaspar Martins , mwakilishi wa Angola kwenye Umoja wa Mataifa akimtambulisha hayati Castro kama mtetezi wa haki asiye na mfano..huku akisema.

(Sauti ya Balozi Martins)

“Alikuwa Fidel ambaye alichangia zaidi kwenye kuimarisha kupatikana kwa uhuru wa Angola pindi nchi hiyo ilipovamia upande wa kaskazini na pia uvamizi mwingine ambao ulikuwa mkubwa zaidi upande wa kusini.”

image
Fidel Castro katika moja ya vikao kwenye Umoja wa Mataifa. (Picha:UN/NICA ID: 143616)
Balozi Martins amesema kama hiyo haitoshi, mara baada ya uhuru, hayati Castro aliridhia kupelekwa kwa walimu nchini Angola ili kuziba pengo na zaidi ya hapo madaktari kutoka Cuba..

(Sauti ya Balozi Martins)

“Wananchi wengi wa Angola wangalipoteza maisha yao kutokana na ukosefu wa matibabu  kama si kwa kuwasili kwa wakati muafaka kwa wataalamu wa afya waliokuwa tayari kufanya kazi kwenye maeneo ya ndani zaidi ya eneo kubwa la Angola kuanzia misitu ya Mayombe hadi jangwa la Namib na eneo lote la uwanda wa mashariki.”