Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yafurahia kuachiliwa huru kwa wafanyakazi wake, Sudan

UNHCR yafurahia kuachiliwa huru kwa wafanyakazi wake, Sudan

Kamishina Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, Filippo Grandi amekaribisha kwa mikono miwili, kuachiliwa huru kwa wafanyakazi watatu wa shirika hilo siku ya Jumatatu , baada ya kushikiliwa mateka kwa karibu mwezi moja kule El Geneina nchini Sudan. Taarifa kamili na John Kibego.

(Taarifa ya Kibego)

Bwana Grandi amewataja wafanyakazi hao kuwa ni Sarun Pradhan, Ramesh Karki na Musa Omer Musa Mohamed waliotekwa nyara tarehe 27 mwezi uliopita.

Amepongeza kwa namna ya kipekee serikali ya Sudan na wahudumu wake waliojitahidi kuhakikisha mateka hao wameachiliwa huru, halikadhalika timu ya Umoja wa Mataifa iliyosimamia kazi hiyo.

Amesema UNHCR, itaendelea kutoa msaada wa kuokoa maisha kwa mamia ya waliokimbia makwao nchini Sudan, huku akitoa wito kwa kila mtu kulinda haki za faragha za walioachiliwa pamoja na familia zao wakati huu mgumu wa kupatiwa tiba ya kisaikolojia.

Adrian Edwards ni msemaji wa UNHCR Geneva.

(Sauti ya Edwards)

''Kama walivyo wafanyakazi wengine wa misaada ya kibinadamu, hawakupaswa kupata mateso ya kutekwa nyara, ukatili na vitisho katika maisha yao, tunazitaka tena pande husika sio tu Sudan bali kila mahali, kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu.''