Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chukueni hatua sasa kuokoa wananchi wa Sudan Kusini- Ban

Chukueni hatua sasa kuokoa wananchi wa Sudan Kusini- Ban

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao kuhusu Sudan Kusini ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema wananchi wamekata tamaa na tegemeo lao lililosalia kwa jamii ya kimataifa linazidi kuyoyoma.

Akihutubia wajumbe wa Baraza hilo Ban amesema ukosefu wa usalama, njaa, uchumi kutwama ni sehemu tu ya madhila yanayokumba wananchi hao licha ya matumaini  waliyokuwa nayo baada ya kupata uhuru mwaka 2011.

Amesema pande kinzani zinavutana ambapo ripoti zinasema kuwa Rais Salva Kiir na wafuasi wake wamepanga mashambulizi dhidi ya kikundi cha SPLM upande wa upinzani ilhali Riek Machar naye wanashamirisha mashambulizi ya kijeshi.

“Wakati sasa umefika kuhakikisha kuwa mkakati wa kusonga mbele unapatia kipaumbele maslahi ya wananchi wa Sudan Kusini na si viongozi.”

image
Wakimbizi wa ndani Sudan Kusini wakisikiliza watoa huduma. (Picha:UNMISS)
Amerejelea wito wake wa kutaka vikwazo vya silaha dhidi ya Sudan Kusini ili kupunguza uwezo wa nchi hiyo kutumbukia kwenye vita na hatimaye wito kwa wajumbe..

(Sauti ya Ban)

“Naliomba Baraza la Usalama lichukue hatua, lichukue hatua sasa ili kukidhi wajibu wake na kusaidia juhudi za kikanda zinazoendelea.”

 

Naye Mkuu wa masuala ya kibinadamu kwenye Umoja wa Mataifa Stephen O’Brien amehutubia baraza hilo kuhusu hali ya kibinadamu akihoji baraza ni ushahidi gani linahitaji ili kuchukua hatua stahiki Sudan Kusini.

Amesema mara kwa mara Baraza limekuwa linasema kamwe halitaki kushuhudia tena yale yaliyotokea Rwanda na Srebenica, lakini kinachoendelea Sudan Kusini hivi sasa ni dhahiri kinataka hatua zaidi badala ya maneno.