Ban akaribisha uundaji wa serikali mpya Lebanon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekaribisha tangazo la kuundwa kwa serikali ya umoja w kitaifa nchini Lebanon.
Katika taarifa kupitia msemaji wake, Katibu mkuu huyo akikaribisha waziri mkuu Saad Hariri amesifu utaratibu mzuri wa mchakato huo huku akiwahimiza viongozi wa kisiasa kuimarisha umoja wa kitaifa.
Ban amemsifu waziri mkuu anayeondoka Tammam Salam kwa uongozi wake.
Halikadhalika amelezea matumaini yake kuhusu serikali hiyo kuhakikisha kwamba uchaguzi ujao utafanyika katika mazingira salama na kwa muda unaokubaliwa na katiba.
Umoja wa Mataifa unatarajia kufanya kazi na serikali mpya ya Lebanon ili kuweza kuangazia changamoto za kisiasa, kiusalama na kibinadamu na kuhakikisha utekelezaji wa maazimio mbali mbali kwa Lebanon ambayo ni muhimu kwa nchi hiyo na eneo hilo kwa ujumla.