Baraza la Usalama laridhia kupelekwa waangalizi Aleppo
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limepitisha azimio ambalo kwalo linaridhia umoja huo kupeleka waangalizi wake kufuatilia uhamishaji wa raia kutoka Mashariki mwa Aleppo.
Likiwa limendaliwa na Ufaransa, azimio hilo namba 2328 lilitanguliwa na mashauriano jana na leo na hatimaye kupitishwa kwa kauli moja.
Azimio linataka Umoja wa Mataifa na wadau wake waendeshe uangalizi usio na upendeleo wowote kwenye kazi ya kuondoa raia kutoka mashariki mwa Aleppo na vitongoji vingine vya mji huo, na wapeleke wafanyakazi kadri wanapohitajika ili haki za raia ziweze kuzingatiwa.
Akizungumzia hatua hii ya leo, mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Samantha Power amesema..
(Sauti ya Samantha)
“Azimio la leo nadhani ni muhimu kwa kuwa angalau hatimaye Baraza limekubali kuwa watu wanaotaka kuondoka Aleppo mashariki wanaweza kufanya hivyo chini ya uangalizi wa Umoja wa Mataifa, Kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu, Chama cha hilal nyekundu cha Syria na wengineo.”
Azimio pia linataka pande husika kwenye mzozo wa Syria kuruhusu bila masharti yeyote Umoja wa Mataifa na wadau wake kuhakikisha misaada ya kibinadamu inawafikia wahitaji kupitia njia ya haraka. Misaada hiyo ni pamoja na mahitaji muhimu kama vile vifaa vya tiba kwa mujibu wa azimio 2258 la mwaka jana halikadhalika azimio linataka pande hizo kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wa misaada na ulinzi wa misafara yao.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anatakiwa kuripoti utekelezaji wa azimio hilo ndani ya siku tano kuanzia leo.