Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanaonyanyasa wahamiaji wawajibishwe- Ban

Wanaonyanyasa wahamiaji wawajibishwe- Ban

Mwaka 2016 umekuwa mwaka wa misukosuko mingi kwa wakimbizi na wahamiaji, wakiendelea kukumbwa na machungu kule wanakotoka na hata wanapokuwa safarini kuokoa maisha yao.

Hiyo ni sehemu ya ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon katika kuadhimisha siku ya wahamiaji duniani hii leo akisema kuongeza chumvi kwenye kidonda hata kule wanakokimbilia bado kuna jamii zinazosaka kuwatenga na hata kuwafukuza wakidai kuwa wanaharibu jamii zao.

Hata hivyo amesema licha ya kiza hicho kilichotanda kwa wahamiaji, bado kuna nuru akitaja azimio la New York la mwezi Septemba mwaka huu kuhusu wahamiaji na wakimbizi ambazo linasaka suluhu endelevu kwa makundi hayo.

Ban amesema sasa ni wakati muafaka kwa serikali zilizoridhia azimio hilo kutekeleza kwa vitendo ahadi zao ili kulinda makundi hayo kwa upendo na kwa kuzingatia haki za binadamu.

Amesema kila mhamiaji ni binadamu mwenye haki za binadamu hivyo ni lazima kukataa sera zozote za chuki dhidi ya wageni na wanaosaka kuumiza wahamiaji wawajibishwe.

image
Wananchi wa Syria wakiwa safarini kusaka hifadhi barani Ulaya. (Picha:Francesco Malavolta/IOM 2015)
Halikadhalika ametaka suluhu la vichochezi vya uhamiaji ambavyo ni pamoja na mizozo, umaskini, ukosefu wa usalam, majanga ya asili na mabadiliko ya tabianchi.

Wakati huo huo Mkurugenzi Mkuu wa shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa William Swing amesema kila uchao ripoti anazopokea kuhusu wahamiaji wanaovuka bahari ya Mediteranea ni za kutia uchungu.

Amesema safari hiyo ngumu na yenye mashaka mwaka huu pekee wa 2016 imekatili maisha ya watu zaidi ya Elfu saba.

Bwana Swing ametoa wito kwa hatua sahihi zichukuliwe ili kusaka suluhu endelevu ya uhamiaji kwa maslahi ya ulimwengu mzima.