Skip to main content

DRC kufunga mitandao ya kijamii Jumapili, Zeid aingiwa na hofu

DRC kufunga mitandao ya kijamii Jumapili, Zeid aingiwa na hofu

Mpango wa serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC kufunga mitandao ya kijamii Jumapili usiku unatia wasiwasi mkubwa, amesema Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein.

Hatua hiyo ya DRC inayoenda sambamba na zuio linaloendelea la maandamano ya mashirika ya kiraia na vyama vya upinzani, linafanyika mkesha wa siku ambayo ni ya mwisho kwa Rais Joseph Kabila kuwa madarakani kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo.

Zeid katika taarifa yake amesema ana wasiwasi kwa kuwa serikali ya DRC imetaka watoa huduma za intaneti na simu kufunga mitandao ya kijamii jumapili usiku akisema kitendo hicho kinaongeza mvutano na waswasi mkubwa.

Ametoa wito kwa serikali kubadili uamuzi huo na kuhakikisha haki ya watu kujieleza na kupata taarifa kwa mujibu wa katiba ya DRC.

Kwa mujbu wa makubaliano yaliyofikiwa na baadhi ya vyama vya upinzani, uchaguzi haufanyiki hadi Aprili mwaka 2018, huku Rais Kabila akipanga kuendelea kuwa madarakani baada ya tarehe 19 mwezi huu ambayo ni Jumatatu.

Mazungumzo yanayoratibiwa na kanisa katoliki nchini DRC yamekuwa yakiendelea mjini Kinshasa kujaribu kusaka suluhu ya mwelekeo wa uongozi baada ya tarehe 19 Disemba ili kuepusha ghasia.