Aleppo ni kisawe cha Jehanam, na jamii ya kimataifa imeshindwa- Ban

Aleppo ni kisawe cha Jehanam, na jamii ya kimataifa imeshindwa- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon leo amefanya mkutano rasmi wa mwisho na waandishi wa habari mjini New York ikiwa ni takribani majuma mawili kabla ya kumaliza awamu ya pili na ya mwisho ya uongozi wake katika chombo hicho .

Katibu Mkuu amezungumzia mambo mseto ambayo Umoja wa Mataifa unayatekeleza  na yaliyokumbwa na changamoto ikiwemo Syria. Amesema suala la Aleppo linamsikitisha sana kwani raia wanauawa, kutoka kwao  inakuwa ni shida huku akifananisha Aleppo na Jehanam.

Halikadhalika mkutano huo ulikuwa na hisia pia pale akitangaza kuwaaga wanahabari ambao amesema ameshirikiana nao ndani na nje ya New York.

( Sauti Ban)

‘‘Ni furaha kubwa kuwaona asubuhi ya leo. Mara nyingi huwa tunakutana kipindi kama hiki katika mwaka, lakini sasa tunakutana wakati wa mwisho wa mhula wangu. Amini usiamini, nitakumbuka nyakati hizi. Tumetumia muda mwingi katika chumba hiki , katika kumbi za jengo hili na duniani kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita

image
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kwenye mkutano wake wa mwicho na waandishi wa habari. Picha: UN Photo/Eskinder Debebe
Kabla ya kujibu maswali ya waandishi wa habari Katibu Mkuu ameizungumzia harakati za makabiliano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi akisema hakuna kurudi nyuma.

(Sauti Ban)

‘‘Tutaendelea kuunga mkono kasi ya dunia katika kusukuma mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi. Hatua zinamaanisha kazi, ukuaji, hewa safi na afya njema. Viongozi kote duniani wanaelewa hili.’’

Miongoni mwa maswali aliyooulizwa Ban ni kuhusu nini kifanyike kuzuia uwezekano wa Sudan Kusini kutumbukia katika mauaji ya kimbari kama ambavyo maafisa kadhaa wa Umoja wa Mataifa walivyotahadharisha.

(Sauti Ban)

‘‘Jumuiya ya kimataifa lazima iingilie kati, kwa kutumia rasilimali muhimu. Najuta sana kwamba nchi wanachama hazijapewa usaidizi kikamilifu na kujihusisha katika kutekelza wajibu huu muhimu wa kulinda kanuni.’’