Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwandishi wa mashairi kutangazwa msanii wa amani

Mwandishi wa mashairi kutangazwa msanii wa amani

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO, Irina Bokova leo anamtangaza mwandishi wa mashairi kutoka Algeria Bi. Ahlam Mosteghanemi kuwa msanii wa amani wa shirika hilo.

Uteuzi wa mtunzi huyo wa mashairi unatokana na utambuzi wake katika vitabu vya utetezi kwa masuala ya haki za kijamii, elimu ya vijana walioathirika na vita, na kujitolea kwake kwa malengo na maadili ya UNESCO

Hafla hiyo inafanyika kwenye makao makuu ya UNESCO huko Paris, Ufaransa.

Bi. Mosteghanemi ni mwanamke wa kwanza kuchapisha mkusanyiko wa mashairi kwa lugha ya kiarabu nchini Algeria ambapo akiwa mwandishi maarufu nakala za vitabu vyake zimeuzwa kwa mamilioni.

Uandishi wake umejenga sio tu fasihi ya Kiarabu na mashairi, bali pia umeongezea kuelewa kwa masuala kama vile ufisadi, dhuluma na haki za wanawake.

Wasanii kwa amani wa kimataifa wa UNESCO hutumika kusaidia shirika hilo kukuza ujumbe na mipango yao.