Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAMID yahofia wafanyakazi wa zamani kukwamisha operesheni

UNAMID yahofia wafanyakazi wa zamani kukwamisha operesheni

Ujumbe wa pamoja Muungano wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa UNAMID huko Darfur hii leo umeelezea wasiwasi mkubwa juu ya majaribio ya hivi karibuni ya mara kwa mara ya wafanyakazi wa zamani wa ujumbe huo ya kutaka kuvuruga operesheni zake.

Taarifa UNAMID imesema kuwa kwa mara kadhaa wafanyakazi kazi hao wamekuwa wakizuia operesheni ndani ya nje ya kambi na wakati mwingine kuzuia wafanyakazi wa UNAMID ambao ni raia wa Sudan kuingia kwenye maeneo ya kazi zao.

Mkuu wa UNAMID Martin Uhomoibhi ambaye pia mwakilishi wa pamoja wa ujumbe huo amesema wanapatia kipaumbele majukumu yao ya kutumikia raia ikiwemo wale watumishi waliomaliza muda wao lakini hawawezi kukubali maandamano yanayofanyika kwa madai ya malipo ambayo amesema hayana msingi wowote.

UNAMID imethibitisha kuwa wafanyakazi wote wa Sudan ambao walimaliza mikataba yao Disemba 31, 2015 walilipwa malipo yao kwa kipindi chote walichohudumu UNAMID, isipokuwa tu kwa kundi ndogo linalosubiri haki za pensheni kushughulikiwa.

UNAMID inashirikiana na ofisi ya Umoja wa Mataifa inayosimamia mafao ya pensheni ili kukamilisha malipo hayo.