Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ulimwengu washuhudia kuporomoka kwa mishahara-ILO

Ulimwengu washuhudia kuporomoka kwa mishahara-ILO

Shirika la Kazi Duniani, ILO limesema kiwango cha mshahara katika nchi zilizoibuka kiuchumi au G20 kimeshuka au kudorora kutoka asilimia 6.6 mwaka 2012 hadi asilimia 2.5 mwaka 2015, na hii imeathiri zaidi ukuaji wa mishahara ulimwenguni kote.

Ripoti ya ILO iitwayo "Ripoti ya Kimataifa ya Mshahara ya mwaka 2016-2017" ambayo imetolewa leo imeonyesha kuwa kiwango cha ukuaji wa mshahara ulimwenguni kimeshuka na kufikia asilimia 1.7, kiwango ambacho ni cha chini zaidi kuwahi kufikiwa katika miaka minne.

Hata hivyo ILO inasema katika mwaka 2015 nchi zilizoendelea kiviwanda zimeshuhudia ongezeko la mshahara katika muongo mmoja.

Ripoti imesema kushuka kwa mshahara kumesababishwa na kushuka kwa bei za bidhaa na mafuta, na vile vile hali ya uchumi uliowasiwasi katika nchi za G20 kama Brazil na Afrika Kusini.

Debora Greenfield, ni Mkurugenzi Mkuu wa sera, ILO na anasema ..

"Tunaona dalili kubwa za kushuka polepole kwa uchumi katika nchi zilizoibuka kiuchumi na zinazoendelea ambazo hapo awali zilikuwa zikiendelea vizuri kabisa".

Halikadhalika ripoti hiyo imeangazia kutokuwepo na usawa katika kipato, ikitolea mfano India ambapo ni asilimia 10 tu ndio wanapata asilimia 43 ya mshahara wa nchi hiyo, ilhali barani ulaya wanaume hupata asilimia 20 zaidi ya wanawake.