Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amina J Mohammed wa Nigeria ateuliwa Naibu Katibu Mkuu wa UM

Amina J Mohammed wa Nigeria ateuliwa Naibu Katibu Mkuu wa UM

Katibu Mkuu mteule wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amefanya uteuzi wa maafisa watatu waandamizi zaidi kwenye umoja huo ikiwemo Naibu Katibu Mkuu ambaye ni Amina J Mohammed wa Nigeria.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric ametaja maafisa wengine waandamizi walioteuliwa kuwa ni Maria Luiza Ribeiro Viotti wa Brazil ambaye anakuwa afisa mkuu  mwandamizi au Chef de Cabinet huku Bwana Guterres akinukuliwa akieleza nia yake ya kuanzisha nafasi ya mshauri mkuu wa sera na kumteua Kyung-wha Kang wa Korea Kusini kushika wadhifa huo.

Kuhusu uteuzi huo wa wanawake watatu kushika nyadhifa hizo za juu zaidi kwenye Umoja wa Mataifa, Bwana Dujarric amemnukuu Katibu Mkuu mteule Guterres akisema..

(Sauti ya Dujarric)

“Nina furaha kutegemea jitihada kubwa za wanawake hawa watatu wenye ujuzi wa hali ya juu ambao nimewachagua kwa kuzingatia ubobezi wao kwenye masuala ya kimataifa, maendeleo, diplomasia, haki za binadamu na usaidizi wa kibinadamu.”

image
Bi. Maria Luiza Ribeiro Viotti wa Brazil , afisa mkuu mwandamizi au Chef de Cabinet. (Picha:UM/# 463227)
Katibu Mkuu huyo ambaye ataanza rasmi majukumu yake tarehe mosi mwezi ujao amesema teuzi hizi za leo ni msingi wa timu  yake ambayo ataendelea kuijenga huku akiheshimu ahadi zake za kuzingatia masuala ya jinsia na tofauti za kijiografia.

Bi. Amina Mohammed ambaye anakuwa mwanamke wa tatu kushika wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kwa sasa ni Waziri wa mazingira wa Nigeria ambapo anachochea jitihada za nchi yake kulinda mazingira na rasilimali kwa maendeleo endelevu.

Kabla ya wadhifa wa sasa alikuwa mshauri maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kuhusu ajenda baada ya mwaka 2015 ambako alikuwa mstari wa mbele kwenye kuundwa kwa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Kwa upande wake Bi. Maria Luiza Ribeiro Viotti kwa sasa anahudumu nchini Brazili kwenye Wizara ya mambo ya nje akijikita kwenye nchi za BRICS ambazo ni Brazili, India, China na Afrika Kusini.

image
Bi. Kyung-wha Kanga, mshauri mwandamizi mteule kuhusu sera. (Picha:UM)
Kuhusu Bi. Kyung-wha Kang kwa sasa ni mkiuu wa timu ya mpito ya Bwana GUterres na ameshika nyadhifa mbali mbali kwenye Umoja wa Mataifa ikiwemo msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kibinadamu tangu mwaka 2013