Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jukwaa la biashara mtandao kwa wote kuzinduliwa Aprili mwakani- UNCTAD

Jukwaa la biashara mtandao kwa wote kuzinduliwa Aprili mwakani- UNCTAD

Kamati ya biashara na maendeleo  ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD imesema mwezi Aprili mwakani itazindua tovuti ya biashara mtandao kwa wote ambamo kwayo watunga sera kutoka nchi zinazoendelea wanaweza kutumia kusaka usaidizi wa kiufundi na kifedha kuboresha biashara hiyo.

Katibu Mkuu wa UNCTAD Dkt. Mukhisa Kituyi amesema kupitia tovuti  hiyo ambayo pia inachagiza usawa wa kijinsia, nchi zinazoendelea zinaweza kunufaika na taarifa na ufahamu kuhusu biashara mtandao na kubadilishana uzoefu na mataifa yaliyobobea kwenye sekta hiyo.

Amesema uzinduzi wa jukwaa hilo la mtandaoni unatokana na ukweli kwamba licha ya biashara ulimwenguni kudororoa kwa miaka kadhaa, biashara mtandao imekua kwa kasi kubwa kutoka thamani ya dola trilioni 16 mwaka 2013 hadi dola trilioni 22 mwaka 2015.

Dkt. Kituyi amesema biashara mtandao imekuwa kichocheo kikubwa cha uchumi, biashara shirikishi na kutoa fursa kwa ajira na amefananisha biashara mtandao na uwezo wa kujua kusoma na kuandika ambapo wale wanaohitaji zaidi bado hawafahamu thamani yake.

Kwa mantiki hiyo amekaribisha hatua ya tume ya Umoja wa Mataifa ya uchumi barani Afrika, UNECA kwa kujiunga na biashara mtandao akisema taasisi zaidi zitajiunga wiki zijazo.