Ushoroba wa kutumia drones kibinadamu waanzishwa Malawi

Ushoroba wa kutumia drones kibinadamu waanzishwa Malawi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF na serikali ya Malawi wametangaza kuanzishwa kwa mara ya kwanza kabisa ushoroba wa kutumia ndege zisizo na rubani au drones kwa ajili ya kusambaza huduma au misaada ya kibinadamu. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

(Taarifa ya Assumpta)

Ushoroba huo wa kwanza barani Afrika ukijikita kwenye huduma za binadamu, utakuwa na urefu wa kilometa 40 unafanyiwa majaribio na utaanza rasmi mwezi Aprili mwakani.

Majaribio hayo yanalenga kufanikisha maeneo makuu matatu ya huduma ikiwemo upigaji wa picha angani kwa shughuli za maendeleo na wakati wa majanga kama vile mafuriko, kuimarisha upatikanaji wa intaneti, na usafirishaji wa vifurushi vidogo ikiwemo vile vya kama vile chanjo na sampuli za damu za wagonjwa.

Mkurugenzi wa ubunifu UNICEF Cynthia McCaffrey mpango huu unaruhusu shirika hilo kuendeleza miradi yake kwa haraka kupitia teknolojia na uwezekano wa kuunganisha matumizi ya drones kwenye huduma za watoto.

UNICEF imesema matumizi hayo yanatoa pia fursa kwa sekta binafsi, vyuo vikuu, na wadau wengine kuchunguza jinsi drones zinaweza kusaidia kutoa huduma hiyo muhimu kwa jamii.