Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo Sudan Kusini ukiingia mwaka wa nne, watoto 17,000 watumikishwa vitani

Mzozo Sudan Kusini ukiingia mwaka wa nne, watoto 17,000 watumikishwa vitani

Zaidi ya watoto 17,000 wanatumika vitani nchini Sudan Kusini tangu kuzuka kwa machafuko nchini humo miaka mitatu iliyopita, limesema leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF. Amina Hassan na taarifa kamili.

(TAARIFA YA AMINA)

Kwa mujibu wa taarifa ya UNICEF, mwaka huu pekee vikosi vyenye silaha nchini humo vimewajumuisha katika vita watoto 1, 300, ambapo tangu mwezi Novemba, visa 50 vya kutekwa na kutumikishwa vitani katika mkoa wa jimbo la Greater upper Nile vimesajiliwa, huku mamia wengine wakielezwa kukumbana na visa hivyo mwezi huu, katika maeneo kadhaa lakini ukosefu wa usalama unasababisha kutothibitisha matukio hayo.

Hata hivyo UNICEF imesema zaidi ya watoto 1900 wameachiliwa katika mikono ya vikosi hivyo, katika kipindi cha mwaka jana na mwaka huu.

Taarifa hiyo pia imeenda mbali kwa kukumbusha pande kinzani nchini, SPLA na SPLA upinzani kuwa zimesaini makubaliano na Umoja wa Mataifa kukomesha na kuzuia utumikishwaji wa watoto vitani.

Wakati huohuo Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir amezindua mchakato wa kitaifa wa maridhiano nchini humo na kuwatolea wito raia akisema.

( Sauti Kiir)

‘Twaweza kufanikisha mambo makuu, ikiwa tutaongea na kujadili masuala yetu kwa amani. Pia nawataka wale wanaofanya propanda na hotuba zenye chuki katika mitandao ya kijamii, kimataifa na kitaifa kuacha kugawanya nchi yao na jamii. Tumeunganishwa kama mtu mmoja, taifa moja, na hatuwezi kuruhusu masuala yakisiasa au kijamii kuharibu umoja wetu.

Kwa ujumla takwimu za madhila dhidi ya watoto zinaonyesha kuwa zaidi ya watoto 2,000 nchini Sudan Kusini wameuawa au kusababishiwa ulemavu, wengine zaidi ya 3,000 wametekwa, na zaidi ya 1,000 wamefanyiwa ukatili wa kingono.