Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuongeze dola bilioni 1 kila mwaka kwa CERF ifikapo 2018 - Ban

Tuongeze dola bilioni 1 kila mwaka kwa CERF ifikapo 2018 - Ban

Katibu mkuu Ban Ki-moon ametoa wito kwa ongezeko wa dola billion moja kila mwaka kwa mfuko wa dharura wa usaidizi wa kibinadamu wa umoja huo CERF ifikapo mwaka 2018.  

Amesema hayo alipohutubia mkutano wa ngazi ya juu kuhusu usaidizi wa kibinadamu kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani hii leo.

Amesema tangu mfuko huo uanzishwe mwaka 2005, umeshatoa dola bilioni 4.6 kwa nchi 98.

Hata hivyo amesema mazingira ya misaada ya kibinadamu ni tofauti na muongo mmoja uliopita akisema mahitaji yameongezeka ikiwa ni watu zaidi ya milioni 65, huku wengi wao wakikosa misaada.

(Sauti ya Ban)

CERF imekuwa na umuhimu zaidi kwa watu walio kwenye migogoro na iliyosahaulika. Ambapo mwaka wa 2016 ilitoa mchango wa dola milioni 150 kwa wale walioathirika kwa kuwapa misaada ya chakula, mazingira tete huko ziwa Chad na wanaokimbia maovu nchini Sudan Kusini

Hata hivyo Ban amesema anajivunia kuanzishwa kwa mfuko huo na mafanikio yaliyopatikana wakati akiwa Katibu Mkuu wa Umoja.

Amezishukuru nchi wanachama 126 na mashirika 43 ya kimataifa na taasisi za kibinafsi kote duniani kwa mchango wao kwa CERF akisema mfuko huo ni chombo muhimu katika nyakati za mgogoro na kwa mafanikio ya ajenda ya 2030 maendeleo endelevu.