Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kujikwamua kutoka kundi la LDCs kwasuasua- UNCTAD

Kujikwamua kutoka kundi la LDCs kwasuasua- UNCTAD

Kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD imesema ni nchi 16 tu kati ya 45 zitaweza kuwa zimejikwamua kutoka kundi la nchi tegemezi, LDC ifikapo mwaka 2021.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya UNCTAD kuhusu nchi hizo ambazo ziko kwenye harakati za kujikwamua kiuchumi ambapo imesema idadi hiyo ni ndogo kuliko lengo la awali.

UNCTAD inasema kujikwamua kunasalia ndoto kutokana na nchi hizo kutumbukia kwenye mlolongo wa utegemezi unaokwamisha ushiriki wao kwenye uchumi wa dunia,  huku ahadi za misaada rasmi ya maendeleo ikisuasua katika utekelezaji.

Mchumi mwandamizi wa UNCTAD Rolf Trager amesema mambo yanayopaswa kuzingatiwa kujikwamua ni pamoja na kuboresha uchumi vijijini, sera bora mtambuka za viwanda, kuimarisha uwekezaji wa umma na kushughulikia suala la ukosefu wa usawa wa kijinsia. Hivyo anasema..

(Sauti ya Rolf)

“Hizi nchi zinapaswa kusaka vyanzo vipya vya ukuaji hasa kwenye soko la ndani lakini pia kwa kuimarisha jitihada zao hasa katika ushirikiano wa kikanda iwe kwa bara la Afrika au Asia.”

Vigezo kwa kujikwamua kutoka LDCs vilianza mwaka 1971 wakati huo kundi hilo likiwa na nchi 49 ambapo ni nchi nne tu hadi sasa zimeweza kufaulu ambazo ni Botswana, Carbo Verde, Maldives na Samoa.

Makadirio yanaonyesha kuwa ifikapo mwaka 2025, kundi la LDCs litakuwa nan chi 32, 30 kati yao zikiwa ni za Afrika, pamoja na Cambodia na Haiti