Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uandikishaji wapiga kura DRC waanza leo

Uandikishaji wapiga kura DRC waanza leo

Kazi ya kutambua na kuandikisha wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao kwenye majimbo 12 ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, imeanza leo.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya uchaguzi, CENI Corneille Nangaa amesema shughuli hiyo imeanza kwenye majimbo manane ya Equateur, Ubangui Kusini, Mongala, Tshuapa, Kivu Kusini, Katanga juu na Lomani Juu.

Amesema kazi hiyo inaenda sambamba na utoaji wa vitambulisho vipya vya wapiga kura.

Uandikishaji kwenye majimbo ya Manyema, Lualaba na Tanganyika utaanza kesho ilhali huko Ituri kinachofanyika kwanza ni mafunzo kwa mawakala wa uchaguzi na kazi ya uandikishaji itaanza wiki ijayo.

CENI imesema wanatarajia kukamilisha shughuli hiyo tarehe 31 mwezi Julai mwakani tayari kwa uchaguzi mkuu mwezi Aprili mwaka 2018.