Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malaria inadhibitiwa Afrika, lakini juhudi zinadorora:WHO

Malaria inadhibitiwa Afrika, lakini juhudi zinadorora:WHO

Shirika la Afya duniani (WHO) kwenye ripoti yake ya mwaka wa 2016 iliyotolewa leo Desemba 13 kwa ajili ya malaria linaeleza kuwa watoto na wanawake wajawazito barani Afrika kusini mwa janga la sahara wana fursa ya kudhibiti malaria. Katika bara zima kwa miaka mitano iliyopita kumearifiwa ongezeko la upimaji  kwa watoto na matibabu ya kuzuia kwa wanawake wajawazito. Na kwa watu wote walio katika hatari ya malaria matumizi ya dawa za kuua mbu na kutumia vyandarua yameongezeka.

Afrika kusini mwa jangwa la Sahara ndiko kunakobeba  mzigo mkubwa wa malaria duniani. Mwaka 2015, eneo hilo lilikuwa na asilimia 90% ya visa vya malaria na asilimia 92% ya vifo vya maradhi hayo huku watoto wa chini ya umri wa miaka mitano wakiwa katika hatari zaidi kwa asilimia 70% ya vifo hivyo. Upimaji unawawezesha wahudumu wa afya kutoa huduma husika haraka na hivyo kuokoa maisha ya mamilioni ya watu.

Tathimini ya ripoti hiyo inaonyesha kuwa takriban asilimia 51% ya watoto waliokuwa na malaria walitibiwa kwenye vituo vya afya vya umma katika nchi 22 za Afrika ikilinganishwa na asilimia 29% kwa mwaka 2010.

Pia ripoti inasema mafanikio hayo yanatokana na watu wengi barani Afrika kutumia vyandarua vyenye dawa katika kujikinga na mbu waenezao malaria. Kwa upande wa tiba pia kumekuwa na ongezeko mara tano hususani kwa wanawake waliopata dozi tatu au zaidi katika nchi 20 za Afrika huku wanaopata chanjo asilimia imeongezeka toka 6% mwaka 2010 hadi 31% mwaka 2015.

Hata hivyo ripoti inasema malaria bado ni jangamoto kubwa kwa huduma za afya ambapo mwaka 2015 kumekuwa na visa vipya milioni 212 na vifo 429,000 kote duniani ambapo katika nchi nyingi, mifumo ya afya yenye rasilimali bado ni hafifu.