Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jukumu la kulinda raia limo kwa serikali

Jukumu la kulinda raia limo kwa serikali

Ni lazima tuanze upya na maisha mapya katika mchakato wa kisiasa nchini Sudan Kusini ili kutengeneza mazingira yatakayoleta amani nchini humo, hayo ni maneno ya Mkurugenzi wa Kitengo cha Afrika katika Operesheni za Kulinda amani kwenye Umoja wa Mataifa, Bwana Michael Kingsley-Nyinah.

Bwana Kingsley-Nyinah akihojiwa na Radio Miraya ya Umoja wa Mataifa wakati wa ziara yake nchini humo amesema kingine kilicho muhimu ni kuhakikisha raia wanalindwa, na hilo sio jukumu la msingi la Umoja wa Mataifa tu, bali pia ni la serikali ya Sudan Kusini kuhakikisha inalinda watu wake. Hivyo akaongeza..

(Sauti ya Michael)

"Nchi hii inatakiwa kutambua utakatifu wa maisha ya binadamu, inatakiwa kutambua kuwa rasilimali ya nchi hiyo imo kwa watu wake, na nchi hii inatakiwa kutambua kuwa- bila ya kujali asili ya kikabila, dini, au mahali pa kuishi- kila Msudani Kusini ana maisha takatifu yanayostahili kuhifadhiwa,kulindwa na kulelewa, na ukiangalia hali jinsi ilivyo,uelewa huo unamomonyoka, na hilo linahitaji ufumbuzi tena."

Amesema suluhu ya amani ya kudumu itapatikana tu ikiwa nchi hiyo itarejelea wingi wa furaha na matumaini yaliyotamalaki wakati wa kuzaliwa kwake.