Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kukomesha ukatili dhidi ya wanawake

Kukomesha ukatili dhidi ya wanawake

Tarehe 25 Novemba dunia imeadhimisha siku ya kimataifa ya kukomesha ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.Maadhimisho hayo yamekwenda sambamba na siku 16 za harakati kote duniani, zinazoanikiza kukomeshwa kwa vitendo hivyo. Siku 16 zinakamilika tarehe 10 Disemba.

Kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na wanawake UN WOMEN, vitendo vya ukatili kwa wanawake ni ukiukaji wa haki za binadmau, huteketeza maisha, husababisha maumivu yasiyoelezeka na pia vina madhara ya kiuchumi.

Takwimu za UN WOMEN zinaonyesha kuwa ukatili dhidi ya wanawake hususani ule unaofanywa majumbani huangusha uchumi kwa kuathiri uzalishaji mathalani nchini Vietnam ambako gharama zinazotokana na vitendo hivyo ni asilimia 1.4 ya pato la taifa.

Nchini Uingereza nako takwimu zinaonyesha kuwa ukatili majumbani kwa mwaka 2009 ulisababaisha hasara ya kiasi cha bilioni 16.

Mapema juma hili wakati wa mkutano kuhusu dhana hiyo mjini Mumbai India, Mkuu wa UN Women Phumzile Mlambo-Ngcuka amesema ukatili dhidi ya wanawake una uhusiano wa moja kwa moja na uwezo wao wa kushiriki katika uzalishaji wa kiuchumi unaoathiriwa kwa kipato kidogo, fursa ndogo za elimu na ajira na ushiriki katika siasa na hivyo akashauri ujuzi na maarifa ikiwemo ujasiriamali utumike kuwezesha wanawake kama njia mbadala ya kuepeka ukatili.

Kufahamu hali halisi ya ukatili dhidi ya wanawake na harakati za kuukomesha barani Afrika , tunamulika Tanzania. Tuungane na Nicolas Ngaiza wa redio washirika Kasibante Fm ya Kagera Tanzania.