Rushwa huchangia ukosefu wa usawa na haki: Ban
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema katika kukabiliana na rushwa inayoongeza kiwango cha umasikini,sekta binafsi na vyombo vya habari vina wajibu mkubwa.
Hii leo Disemba tisa, 2016 ni siku ya kimataifa ya kupinga rushwa.
Akizungumza wakati wa utolewaji wa tuzo za kupinga rushwa zenye jina la Mfalme wa Qatar Sheikh Tamim Bin Hamad Al Thani, zilizofanyika mjini Vienna Austria, Ban amesema licha ya kwamba jamii nzima inapaswa kuhusika katika makabiano dhidi ya rushwa, sekta binafsi na vyombo vya habari vina wajibu mkubwa katika kuhakikisha uwajibikaji, uaminifu na uwazi.
Amesema pale uaminifu unapovunjika katika jamii, ubinafsi hutawala ambao ni kichocheo kikubwa cha ukosefu wa usawa na haki.
Akisisitiza Katibu Mkuu amesema makabiliano ddidi ya rushwa yana msingi katika lengo namba 16 la maendeleo endeleveu SDGs linalotaka jamii yenye amani,jumuishi na inayopunguza rushwa.
Ban ameongeza kuwa ikiwa lengo hilo litatekelezwa jamii itakuwa yenye usawa na haki hususani kwa wanawake na wasichana.