Skip to main content

Ombi la dharura kuhamisha majeruhi kutoka Aleppo

Ombi la dharura kuhamisha majeruhi kutoka Aleppo

Kwa mara nyingine tena suala Syria limejadiliwa wakati wa kikao cha faragha cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo wajumbe wamepata taarifa kutoka kwa mjumbe maalum wa Umoja huo nchini Syria, Staffan de Mistura.

Akizungumza na wanahabari baada ya kikao hicho, Bwana de Mistura amesema pamoja na mambo mengine Urusi imezungumzia usitishaji wa mapigano kutoka vikosi vyao na vile vya serikali huko Syria ili kuwezesha raia kuondoka kwa hiari maeneo ya mapigano.

Amesema hajafahamu sitisho hilo ni kwa muda gani na alipoulizwa raia hao wataenda wapi wakitoa Aleppo, Bwana de Mistura amesema..

 (Sauti ya de Mistura)

“Jumamosi ni siku ambayo imekuwa inajadiliwa Geneva.. lakini wataelekea wapi? Ni moja ya hoja ninazofahamu lakini sitajadili kabla warusi na wamerekani watajadili jumamosi na jumapili mjini Geneva.”.

Bwana de Mistura amesema kwa mtazamo wake kikao cha leo kilikuwa na umoja miongoni mwa wajumbe akisema pengine inatokana na suala kwamba wajumbe wametambua ni nani wanaotaabika kwenye zahma inayoendelea.

image
Mtoto akiwa mbele ya jengo la shule lililobomolewa huko Aleppo. (Picha:© UNICEF/UN018873/AlshawiSyrian Arab Republic, 2016)
Awali kutoka kikao cha kikosi kazi cha kimataifa kuhusu Syria, Umoja wa Mataifa umesema kuna hali ya kukata tamaa kutoka Aleppo, ambako watu wanataka majeruhi wahamishwe kutoka eneo hilo.

Mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa Jan Egeland amewaambia waandishi wa habari kuwa kinachotakiwa sasa ni sitisho la mapigano na misaada iweze kufikia wahitaji, na majeruhi waweze kuhamishwa wakati huu ambapo zaidi ya watu 30,000 wameshakimbia kutoka maeneo yanayoshikiliwa na vikosi vya serikali huko Aleppo.

(Sauti ya Egeland)

 “Tumepokea maombi ya dharura kutoka ndani ya Aleppo.. tumefikishiwa sisi kama binadamu, watoa huduma za kibinadamu, kutoka kwa madaktari, mashirika ya kiraia na wote wanatueleza kuhusu hali ya kukata  tamaa na umuhimu wa kuhamisha watu eneo hilo.”