Takribani robo ya watoto duniani wanaishi kwenye mizozo- UNICEF

9 Disemba 2016

Zaidi ya watoto milioni 535 duniani wanaishi kwenye nchi zilizokumbwa na mizozo au vita. Hiyo ni kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, ikiwa ni taarifa iliyotolewa leo kuelekea maadhimisho ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwa chombo hicho kinachomulika ustawi wa watoto.

UNICEF imesema idadi hiyo ni sawa na mtoto mmoja katika kila watoto wanne ambapo robo tatu wako nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara, wakiwa hawana huduma za tiba, elimu bora, lishe sahihi na ulinzi.

Akizungumzia takwimu hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Anthony Lake amesema zinakumbusha jukumu la jamiii ya kimataifa kupatia udharura suala hilo kila siku kwani vita, majanga asilia ikiwemo mabadiliko ya tabianchi yanaweka watoto katika hatari ya kupata magonjwa, kutumikishwa na kunyanyaswa.

Amesema dharura zinazokumba watoto walio hatarini zaidi dunia hivi sasa zinatishia mafanikio yaliyopatikana miongo ya karibuni ikiwemo kuongezeka kwa idadi ya watoto wanaokwenda shuleni.

Hata hivyo amesema licha ya mazingira ya mizozo, maendeleo ya mtoto ni muhimu bila kujali yuko vitani au la.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter