Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haki za binadamu ziko katika shinikizo kubwa duniani kote: Zeid

Haki za binadamu ziko katika shinikizo kubwa duniani kote: Zeid

Shinikizo kubwa katika viwango vya kimataifa vya haki za binadamu linahatarisha kuvuruga mipango ya ulinzi iliyowekwa baada ya mwisho wa vita ya pili ya dunia , amesema Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein.

Akizungumza katika kuelekea siku ya haki za binadamu inayoadhimishwa kila mwaka Desemba 10, Zeid pia amesisitiza kwamba ni jukumu la kila mtu kuwajibika katika kuepuka shinikizo hilo na wengi tayari wanafanya hivyo.

Zeid amesema mwaka 2016 umekuwa mbaya sana kwa haki za binadamu kote duniani na endapo mmomonyoko wa mifumo ya haki za binadamu na utawala wa sharia itaendelea kushika kasi , basi hatimaye kila mtu ataathirika.

Amesema viongozi wanashindwa kukabiliana kwa uaminifu na ufanisi masuala magumu ya kijamii na kiuchumi, hivyo watu wanageukia katika kukata tamaa na kutumia hofu, kupanda mgawanyiko, na kutoa ahadi wasizoweza kutimiza.

Kamishina mkuu amewataka watu wote kote duniani kutetea mfumo uliowekwa kwa lengo la kuifanya dunia kuwa mahali bora kwa kila mtu.