Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wanaohamahama wanahitaji ulinzi wa dharura- UNHCR

Watoto wanaohamahama wanahitaji ulinzi wa dharura- UNHCR

Kila uchao, makumi ya maelfu ya watoto duniani kote wanakimbia makwao kutokana na mapigano, ukosefu wa usalama na hata mateso na kulazimika kukimbilia ugenini au kusalia wakimbizi ndani ya nchi yao, ulinzi ukiwa mashakani.

Hiyo ni kauli ya Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi Filipo Grandi wakati mjadala wa tisa kuhusu ulinzi wa watoto. Rosemary Musumba na ripoti kamili.

(Taarifa ya Rosemary)

Katika mjadala huo wa siku mbili unaofanyika Geneva, Uswisi kujadili udharura wa kulinda watoto, Bwana Grandi amesema watoto wanalipa gharama za ukosefu wa utashi wa kisiasa duniani katika kuzuia na kutatua mizozo na hata kupunguza madhara yake.

Amesema mazingira hayo yameweka watoto zaidi ya milioni 28 duniani kote kusalia wakimbizi, vitendo vya ukatili dhidi yao vikiwa vimewazingira.

Hivyo kamishna huyo mkuu wa UNHCR amesema..

(Sauti ya Grandi)

“Hatuwezi kukubali hili! Lazima tuchukue hatua kwa kuwa hali hiyo inaweza kuwatumbukiza watoto siyo tu kwenye utumikishaji bali pia kupata misimamo mikali hasa kwenye maeneo ya pembezoni huko Ulaya ambayo yanaweza kuwa chemchem ya mienendo hatari.”